(ABNA24.com) Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Sabri Boukadoum wamebainisha hayo Jumanne usiku katika mazungumzo ya simu ambapo wametathmini matukio ya hivi karibuni ya Ulimwengu wa Kiislamu na kusema mpango muovu wa 'muamala wa karne' ni wa kidhalimu na unapingwa.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Algeria aidha wamesisitiza kuhusu ulazima wa kuunga mkono haki za watu wa Palestina.
Jana usiku pia Zarif alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kusisitiza kwamba, Iran ipo pamoja na taifa la Palestina na inaunga mkono haki za taifa hili likiwemo suala la kuundwa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa Baitul-Muqaddas.
Katika mazungumzo yake hayo na Mahmoud Abbas, Dakta Zarif amelaani pia mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne na kusema kuwa, Iran inafanya juhudi katika siasa zake kuhakikisha kuwa, katika mustakabali inazuia kufikiwa mipango na njama kama hizi dhidi ya wananchi wa Palestina.
Wiki iliyopita, Rais wa Marekani, Donald Trump alizindua mpango wa Muuamala wa Karne akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa utawala bandia wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Kwa mujibu wa mpango huo, Quds Tukufu itakabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni; wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki tena ya kurejea katika ardhi za mababu zao na Palestina itamiliki tu ardhi zitakazosalia huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.
..........
340